Home MAKALA CCM Kinavyoziishi Ndoto za hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

CCM Kinavyoziishi Ndoto za hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

477
0

CCM kimeanza kufufua vyuo vilivyowafunza makada wake uongozi, siasa na itikadi, ambavyo vilikufa miaka 20 iliyopita.

Vyuo hivyo vilianzishwa na hayati baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kufuatia ushauri wa Tume ya Amoni Sekela (Mwaka 1965), kuhusu umuhimu wa mfumo wa siasa za chama kimoja.

Lengo lilikuwa kupata viongozi wazalendo, kwenye siasa za chama kimoja chenye itikadi za ujamaa na kujitegemea.

Vilianzishwa vyuo vya Ihemi-Iringa, Tunguu-Zanzibar, Tunguru-Sengerema, Murutunguru – Ukerewe, Mahiwa-Kanda ya kusini, Hombolo-Dodoma, Ilonga-Kilosa na Kivukoni – Kigamboni, jijini Dar es salaam.

Walengwa wa mkakati huo walikuwa viongozi wa serikali, wa chama, watumishi wa umma na viongozi wastaafu, ambao walijengewa uwezo wa kuchukia kuomba omba na kutotegemea kuajiriwa bali kujiajiri.

Hata hivyo kwa nyakati tofauti ubora wa vyuo hivyo uliporomoka, mpaka kufikia Mwaka 1999, vingi vilikufa vikageuka magofu na mapori huku vyuo vya Hombolo, Ilonga na Kivukoni vikitwaliwa na serikali.

Ndoto Zinavyofufuliwa:

Safu ya Viongozi wa CCM, Awamu ya Tano.

Safu mpya ya uongozi wa CCM chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, mwezi huu imezindua Chuo cha Ihemi ambacho kilikufa tangu Mwaka 1999.

Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara, Philip Mangula akiongozana na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally pamoja na viongozi wengine wengi wa chama na serikali, walitekeleza jukumu hilo hivi karibuni.

Udahili wa wanafunzi chuoni hapo utaanza Janari, 2020 na Makamu Mwenyekiti Mangula aliwaasa watakaopata fursa hiyo kubadilika kifikra, ili badala ya kung’ang’ania kuajiriwa wajiajiri kupitia sekta ya kilimo.

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Kayanza Pinda, akiwa mmoja wa viongozi walioshiriki uzinduzi huo alieleza kufurahishwa na tukio hilo, akisema litaongeza viongozi na au wastaafu vinara wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa kuwekeza katika sekta ya kilimo na viwanda.

Dkt. Bashiru, alitangaza bodi ya muda itakayoshauri namna ya kuendesha vyuo hivyo, wakati utaratibu rasmi wa kuviendesha ukiandaliwa na Kamati Kuu ya CCM.

Alitaja baadhi ya viongozi wa chama hicho, kwa vyeo siyo majina yao kwamba wataunda bodi hiyo, ambayo itakuwa chini ya Katibu Mkuu wa CCM.

“Bodi hii itaundwa na  mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa ambaye atakuwa mwenyekiti wa bodi, mkuu wa chuo atakuwa katibu, mlezi wa chama wa mkoa atawakilisha kamati kuu kwenye bodi, Wajumbe wa bodi watakuwa Mnec wa Iringa, makatibu wa  jumuiya wa mkoa na mlezi wa jumuiya na Idara ya Itikadi ya Uenezi itatakiwa kuteua mtu mmoja, atakayeingia kwenye bodi hii ya chuo,” alielekeza Dkt. Bashiru.

Dkt. Bashiru pia aliweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa ukumbi wa chuo na alikagua miradi ya maendeleo ya chuo hicho, ikiwemo vitalu vya nyanya na mboga mboga.

Chuo kitakuwa na miradi 21 na mpaka sasa, baadhi imekamilika ikiwa imegharimu jumla ya Sh. Mil. 846.28 na kitatoa ajira zaidi ya 14000.

Katika hatua nyingine mapema mwakani CCM kitazindua chuo kingine cha aina hiyo cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha, chenye hadhi ya kimataifa.

Kitatoa mafunzo hata kwa wanachama wa vyama rafiki, vya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole sendeka, alipongeza utekelezaji wa mkakati huo kwamba unamuenzi hayati baba wa taifa kwa vitendo.

Mkakati huo pia utaongeza watu wenye ari ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda, hivyo kutimiza ndoto za Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye  anataka Tanzania yenye amani na mshikamano isiyoyumbishwa na mabeberu.

Na Said Said Nguya, Makao Makuu ya CCM, Dodoma.