Home Habari HATMA YA MHADHIRI ANAYETUHUMIWA RUSHWA YA NGONO UDOM, MIKONONI MWA DPP.

HATMA YA MHADHIRI ANAYETUHUMIWA RUSHWA YA NGONO UDOM, MIKONONI MWA DPP.

339
0
DPP BISWALO MGANGA.

Sakata la Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jacob Nyangusi anayetuhumiwa kudai rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake (jina linahifadhiwa), limetua mezani kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kesi katika Ofisi hiyo, Hashim Ngole, katika mazungumzo maalumu na chombo hiki amethibitisha, lakini hakuwa tayari kulizungumzia kwa kina kwasababu mwenye mamlaka hayo ni DPP.

“Kweli jalada tunalo, tunaendelea kulifanyia kazi lakini kama unahitaji taarifa za kina siwezi kukupatia kwasababu mwenye mamlaka hayo ni DPP, labda akiniruhusu kufanya hivyo,” amesema Ngole.

Sheria Namba 3 ya Mwaka 2016 aya ya 21 kwenye jedwali la kwanza la Sheria ya Uhujumu uchumi, makosa yote ya rushwa yamewekwa kuwa ya uhujumu uchumi isipokuwa ya kifungu cha 15.

Hiyo inamaanisha, watuhumiwa wa makosa yote ya rushwa isipokuwa ya kifungu cha 15 ili wafikishwe mahakamani lazima kipatikane kibali cha DPP. Kibali hicho kinatakiwa kutolewa ndani ya siku 60 tangu jalada lifikishwe kwa DPP.

Takukuru ngazi ya mkoa baada ya kukamilisha wajibu wake, hupeleka jalada makao makuu ya taasisi hiyo ambako nako baada ya kulishughulikia, huwasilishwa kwa DPP ili kupatiwa kibali.

Mkurugenzi Ngole alisema mahakama kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, DPP akijiridhisha mashtaka yamekidhi vigezo, hutoa kibali ili hatua za kimahakama ziendelee.

Pia anaweza kutoa kibali kinachoipa mahakama nyingine mamlaka, mfano mahakama ya mkoa, kusikiliza kesi ya aina hiyo. Au akibaini mianya inayoweza kuharibu kesi, anaweza kurejesha jalada kwa mamlaka zilizolifikisha kwake akielekeza mapungufu husika yafanyiwe kazi.

DPP pia ana mamlaka ya kufuta mashtaka yoyote endapo ataona kwa kufanya hivyo, maslahi ya umma yatakuwa yamelindwa.

Mwanzo wa Sakata Hili:

Oktoba 4 mwaka jana, Nyangusi alikamatwa na Takukuru Saa 3:00 usiku kwenye chumba cha kulala, nyumbani kwake eneo la nyumba Miatatu, Kata ya Nzuguni jijini Dodoma akiwa na mwanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza (jina linahifadhiwa).

Mkuu wa Takukuru wa Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, aliueleza umma kuwa awali walipata taarifa zikimtuhumu mhadhiri huyo kwamba alikuwa akimtaka kingono mwanafunzi huyo, kama sharti la kumfaulisha mtihani wa somo analofundisha.

Baada ya kupeleleza na kubaini ukweli wa taarifa hizo, alisema waliweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwake na sasa mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana.