Home Dodoma TARURA: “TUTAIFUMUA” NZUGUNI

TARURA: “TUTAIFUMUA” NZUGUNI

378
0

Mvua za masika zimeanza kusababisha mafuriko Nzuguni, kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini.

Baadhi ya watu wameshindwa kuingia au kutoka kwenye baadhi ya mitaa kwa saa kadhaa, huku baadhi wakishuhudiwa wanavuka daraja linalounganisha Mtaa wa Nzuguni C na B lililofunikwa na maji, jambo ambalo ni hatari.

HALI ILIVYOKUWA KWENYE DARAJA LINALOUNGANISHA MITAA YA NZUGUNI C NA B

Eneo hilo ni moja kati ya mengi korofi, kwenye barabara za mitaa ya Kata ya Nzuguni.

Meneja wa Wakala wa Barabara wa vijijini na mijini (Tarura) wa Jiji la Dodoma, Mhandisi Geofrey Mkinga, kwa niaba ya Mratibu mamlaka hayo wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Lusako Kilebwe, amesema hatua za utatuzi wa changamoto hizo zimeanza kuchukuliwa.

“Tofauti na wananchi ambao ili wajue mradi umeanza mpaka mkandarasi aonekane “site” (eneo la kazi), kwetu wataalamu mradi huanzia kwenye maandalizi,” amesema Mhandisi Mkinga.

Ameitaja Nzuguni kuwa moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, kutokana na kuwepo njia mbadala ya kuelekea Ikulu.

Hii ni barabara inayochepuka kutoka barabara ya Morogoro-Dodoma, kwenye eneo linakojengwa soko kuu na stendi kuu ambayo inaelekea Nzuguni na kuunganisha Mitaa ya Mahomanyika, mji mpya wa serikali mpaka Ikulu.

MKURUGENZI WA JIJI LA DODOMA, GODWIN KUNAMBI

Kwa mujibu wake, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 11 inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Barabara nyingine zinazounganisha mitaa ya kata hiyo amesema zitafanyiwa matengenezo  ikiwamo kujenga mitaro ya kusafirisha maji ya mvua kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kulingana na ushauri utakaotolewa na wataalamu.

CHANGAMOTO

Mhandisi Mkinga amesema ujenzi usiyozingatia sheria na taratibu za mipango miji, ambao umefanywa kwenye maeneo mengi ya Kata hiyo ni changomoto katika kuweka mifumo ya maji ya mvua na maji taka.

Kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi wamepata mkandarasi msanifu, Chiel Enginearng Co. Ltd kwa kushirikiana na Joma Consult Ltd; anayefanya utafiti kwenye maeneo hayo ili ashauri namna nzuri ya kutoa maji ya eneo hilo.

Amesema Nzuguni na baadhi ya maeneo ya Ilazo yapo chini, maji ya mvua yanayotoka kwenye maeneo mengi ya Jiji huelekea huko ilhali hakuna mzunguko mzuri wa kuyaondoa.

Mtaalamu huyo mshauri ambaye tayari anafanya utafiti, anatakiwa kukamilisha mapema, ili bajeti ya fedha za kutekelezea mpango huo, iwasilishwe kwenye Bunge la Bajeti lijalo, Aprili mwakani.  

Mhandisi Mkinga amesema TARURA kama ilivyokuwa mwaka jana, hata msimu huu inatarajia kufanya matengenezo ya kawaida kwenye baadhi ya maeneo ya barabara za Nzuguni, ili kuwapunguzia adha wananchi.