Home Habari DKT. BASHIRU ASEMA WALIOIBUKA NA KAULI “KAZI NA BATA” NI WASALITI

DKT. BASHIRU ASEMA WALIOIBUKA NA KAULI “KAZI NA BATA” NI WASALITI

321
0

NA SAID SAID NGUDA.

KATIBU MKUU WA CCM, DKT.BASHIRU ALI

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, amewaomba wananchi kupuuza sera na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini zikiwataka wale bata (wastarehe) badala ya kufanya kazi.

Dkt. Bashiru amesema kiongozi kutoa kauli za aina hiyo ni usaliti wa mapambano ya kiuchumi, yanayahimiza kitaifa.

Dkt. Bashiru alikuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya CCM ya Kata ya Bwanjai, wilayani Misenyi ambapo pia alizungumza na wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi.

“Tunaongoza mapambano ya kujikomboa kiuchumi, kila mtu kwa nafasi yake anatakiwa kuhimiza kufanya kazi kwa bidii, kama CCM inavyotumika kauli mbalimbali ikiwamo hapa kazi tu, kazi na maendeleo, Uhuru na kazi na kazi ni utu, ila kuna baadhi ya vyama vinahubiri kazi kwa starehe,’’ amesema Dkt. Bashiru na kuendelea

“Unaposema kazi na bata, ni kudharirisha wanawake na mama zetu ambao wamekuwa wakifanya kazi ili wasomeshe watoto, walishe familia na sote ni matokeo ya juhudi zao kubwa, kuwambia wale bata ni sawa na kuwataka waache majukumu hayo na kuishia kwenye starehe…, ni kauli za kipumbavu za vyama vya uchaguzi tunatakiwa kuzidharau na kuzipuuza,” alisema.

Akizungumzia hotuba ya Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Magufuli, katika ufunguzi wa semina ya waNEC Desemba 12, 2019 na ile ya Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Ali Mohammed Shein wakati akifunga semina hiyo, alisema zote zinahimiza maendeleo ya viwanda ambayo yatafanya vijiji kuwa vitovu vya maendeleo, kwani msingi wa viwanda ni kilimo.

Amesema CCM kitaendelea kutetea haki za wanyonge na kitahakikisha hata sekta zote za serikali, zinaendelea kutoa huduma kwa wananchi bila usumbufu wala ubaguzi.

Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye alisema ingawa ujenzi wa mradi huo unakwenda taratibu kutokana na majukumu kuingiliana na mchakato wa uchaguzi, atahakikisha jengo hilo linakamilika.

Pamoja naye, viongozi mbalimbali wa CCM na wa serikali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanal mstaafu Denis Mwila walihudhuria tukio hilo. Dkt. Bashiru, yupo kwenye mapumziko nyumbani kwake Bukoba, mkoani Kagera mpaka Januari mwaka.