Home Dodoma BENJAMIN MKAPA HAIKAMATIKI KATIKA TIBA ZA FIGO

BENJAMIN MKAPA HAIKAMATIKI KATIKA TIBA ZA FIGO

529
0
MKURUGENZI MTENDAJI WA BMH, DKT. ALPHONCE CHANDIKA, AKIFAFANUA JAMBO KWA WANAHABARI JIJINI DODOMA LEO.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Chuo Cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), imenusuru takriban Sh. 1.1 bilion kwa kupandikiza figo kwa wagonjwa 11.

Mpaka sasa jumla ya wagonjwa 22 wamepatiwa tiba ya figo hospitalini hapo, kwa maana ya waliopandikizwa figo 11 na wale ambao walijitolea kuwapatia figo ndugu zao 11.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Alphonce Chandika amesema kwasasa timu ya wataalamu 13 wa kitanzania wamefanikiwa kupandikiza figo kwa wagonjwa wanne, chini ya uangalizi wa timu ya wataalamu Kumi kutoka Tokushukai Medical Group na Tokyo Women’s Medical University, wa nchini Japani.

“Wataalamu hawa wageni wamejiridhisha na kututhibitishia kuwa wataalamu wetu wa nchini wana uwezo wa kutoa tiba hii bila kusimamizi, tunawashukuru sana kwasababu badala ya kutupatia samaki, wametufunza namna ya kuwavua na tumefuzu,” amesema.

Amesema serikali ilikuwa ikitumia wastani wa Sh. 100 milioni kwa kumpatia mgonjwa mmoja tiba ya kupandikizwa figo nje ya nchi, kwa maana ya kuhudumia mgonjwa anayepandikizwa na yule anayejitolea figo lakini sasa huduma hiyo inatolewa hospitalini hapo kwa wastani wa kati ya Sh. 22 hadi 25 milioni kwa tiba ya mgonjwa mmoja.

Naye Mkuu wa Chuo Cha Tiba cha UDOM, Profesa Ipyana Mpagatwa, amesema uhusiano kati ya taasisi hizo za Japani na UDOM ulianzishwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa miaka Kumi iliyopita ambapo Mwaka 2012 urafiki huo ulifanikisha kuanzishwa huduma ya kusafisha damu kwa watu wenye matatizo ya figo.

DKT. CHANDIKA (KUSHOTO) AKIWA NA MKUU WA CHUO CHA TIBA CHA CHUO KIKUU CHA DODOMA (UDOM), PROF. IPYANA MPAGATWA KWENYE MKUTANO NA WANAHABARI LEO, JIJINI DODOMA.

“Baadaye Mwaka 2016 tukaanza kutoa tiba hii ya kupandikiza figo baada ya wataalamu wetu kupatiwa mafunzo na wataalamu hawa, hapa nchini na wakati mwingine wataalamu wetu wakilazimika kwenda Japan, tunashukuru kwamba sasa wamefuzu kwa kiwango cha kuachwa waendelee kutoa tiba bila usimamizi wa karibu,” amesema.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya figo wa BMH, Dkt. Kessy Shija, amewahakikishia watanzania kuwa wapo vizuri kitaalamu na hata kwa vifaa tiba kuwahudumia wale wote wanaopatwa na magonjwa ya figo.

“Hawa wataalamu tumekuwa nao kwa muda usiyozidi wiki moja, hiyo inamaanisha kuwa huu upasuaji wa wagonjwa wanne maandalizi yake tumeyafanya wenyewe na yamefanikiwa kwa asilimia 100, hata upasuaji kwa maana ya waliotoa na waliopandikiziwa figo tumefanya wenyewe na umefanikiwa kwa asilimia 100,” amesema Dkt. Shija.

Kwa mujibu wa Daktari bingwa huyo, kwa mara ya kwanza nchini, hospitali hiyo imefanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa ambaye amekuwa akiachwa kutokana na kinga yake ya mwili kuwa juu,

BAADHI YA WATAALAMU WA KUPANDIKIZA FIGO BMH. WAKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA NA WATAALAMU KUTOKA NCHINI JAPAN

“Kinga ya mwili wa mgonjwa inapokuwa juu akipandikizwa figo nayo inawezakufa hivyo tumeweza kupunguza kinga zake na tukamfanyia upasuaji wa kupandikiza figo, mpaka sasa anaendelea vizuri kabisa,” amesema Dkt. Shija.

Amesema inawezekana kwenye hospitali nyingine nchini wameweza kukutana na changamoto hiyo na kukabiliana nayo kwa namna tofauti, lakini hakuna haikuwahi kutokea changamoto ya wingi wa kinga ikatatuliwa kwa kuanza kushughulikia kinga na ndipo upasuaji ukafanyika, kama walivyofanya wao.