Home Dodoma HAKUNA BIASHARA YA VIUNGO VYA BINADAMU TANZANIA

HAKUNA BIASHARA YA VIUNGO VYA BINADAMU TANZANIA

329
0
LEAH KISHOSHA

Dhana kwamba unaweza kuuza kiungo chako kwa anayekihitaji kwa ajili ya tiba, kwamfano figo, ni dhana potofu kwasababu sheria nchini hairuhusu biashara hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Alphonce Chandika amesema kabla mgonjwa hajapadikiziwa figo, kuna taratibu nyingi zinazingatiwa ili kuhakikisha anayejitolea anafanya hivyo kutokana na upendo na siyo vinginevyo.

Amesema pia kuna kamati maalumu mabayo hufanya mahojiano na mgonjwa, familia yake pamoja na anayejitolea kumpa mgonjwa figo, ili kujiridhisha kwamba hakuna biashara iliyofanyika.

MKURUGENZI MTENDAJI WA BMH, DKT. ALPHONCE CHANDIKA, AKIFAFANUA JAMBO MBELE YA WANAHABARI, JIJINI DODOMA.

Pia mgonjwa na aliyejitolea kumpa figo, hupimwa ili kuhakikisha kuwa vinasaba vyao ni sawa na kwamba kwa msingi huo, anayetoa hutakiwa kuwa ndugu wa karibu wa mgonjwa.

Mmoja kati ya watu 22 ambao mpaka sasa wameondolewa na kupandikiziwa figo kwenye hospitali hiyo, Leah Kishosha, amesema alipata tatizo la figo kutokana na kuugua kisukari na shinikizo la damu (presure).

Amethibitisha hakuna biashara ya kiungo hicho kwakuwa ameshuhudia matajiri, wakifariki kwa kukosa watu wa kuwapatia figo na kwamba kama zingekuwa zinauzwa, bila shaka wangenunua.

“Kuna mwanaume alikuwa mfanyabiashara mkubwa hapa Dodoma (bila kumtaja jina), tulikuwa tunakutana BMH kwenye tiba ya kusafishwa figo, amefariki kutokana na ndugu, watoto wake kukataa kumpa figo…, ingekuwa zinauzwa angenunua kwasababu hela alikuwa nayo ya kutosha tu,” amesema Leah.

Kwa upande wake amesema dada zake wawili wote walijitolea kumpa figo, lakini uchunguzi ulibaini mmoja figo yake ina mishipa mitatu ya damu wakati yakwake ina mishipa miwili, sawa na dada yake aliyemtaja kwa jina la Eunice, ambaye ndiye aliruhusiwa kumpa msaada huo.

Kwa mujibu wa Dkt. Chandika, Mwaka 2018 hadi 2019 BMH walipandikiza figo kwa wagonjwa Saba na Januari 6 mpaka 7 mwaka huu, wengine wanne walipatiwa tiba hiyo hivyo kufanya jumla ya wagonjwa 22 waliopatiwa tiba hiyo hospitalini hapo.

Idadi hiyo inajumuisha wagonjwa 11 waliofanyiwa upasuaji ili kuondolewa figo na wengine 11 kufanyiwa upasuaji ili kupandikiziwa figo.

Amesema wagonjwa wote hao wanaendelea kuishi vizuri, wakiwa na afya nzuri kabisa na kusisitiza, hakuna biashara ya viungo vya binadamu nchini Tanzania.