Home Habari PROF. MCHOME ATAKA TUMESHERIA IENDELEZE WATUMISHI WAKE KITAALUMA

PROF. MCHOME ATAKA TUMESHERIA IENDELEZE WATUMISHI WAKE KITAALUMA

258
0
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome, akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA wakati wa Uzinduz wa Baraza hilo.

NA KARIMU MESHACK,

NGORONGORO

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome ameiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, kuboresha maslahi ya watumishi wake, ikiwamo kuwaendeleza kitaaluma ili kuongeza ufanisi kazini.

Amesema hayo kwenye uzinduzi wa Baraza jipya la Wafanyakazi wa Tume hiyo na kuitaka menejimenti ya TUMESHERIA kuweka utaratibu wa kutambua mchango wa watumishi wanaotekeleza majukumu yao vizuri zaidi, hivyo kuwa chachu katika maendeleo ya tume na serikali kwa ujumla.

Nalo Baraza la Wafanyakazi limeagizwa kuweka mazingira mazuri, yatakayoruhusu mwajiri kuwajengea uwezo watumishi, ikiwamo mpango wa Mafunzo.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA wakiteta jambo na Kiongozi wao Bi. Sifrosa Mmari (kushoto)muda mchache kabla ya Uzinduzi wa Baraza hilo.

Ameasa kuwa Baraza hilo linatakiwa kuwa mdau na mshirika wa tume na serikali, kwa kubuni mbinu mpya za uendeshaji na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Katika kufanya hayo, Baraza limetakiwa kulenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuimarisha uhusiano wa kiutendaji, baina ya watumishi na menejimenti na siyo kupokea malalamiko ya wafanyakazi pekee.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Casmir Kyuki, amesema wamefanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo, wameandaa Mpango wa Mafunzo na Urithishwaji wa Madaraka (Succession Plan) ili kuwaongezea uwezo watumishi wao.

“Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, tuliwezesha watumishi Saba wa kada tofauti kupata mafunzo kuhusu kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao (TANEPS), kuandaa Mipango na Bajeti  na uandaaji wa mfumo mpya wa Neno Kuu (Key Word Filling Classification System) wa utunzaji wa   kumbukumbu,” amesema Kyuki na kuendelea,

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria (katikati), na Viongozi wa Baraza la Wafanyakazi na Menejimenti ya TUMESHERIA baada ya Uzinduzi.

“Lengo la hatua hiyo ni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu hayo ndani ya Tume na hata sehemu zingine serikalini, tukiamini kwa kufanya hivyo tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika kuiletea Tanzania maendeleo ya uchumi wa kati na waviwanda.”

Uzinduzi huo wa Baraza jipya umefanyika kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA, kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Mkuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo pamoja na mambo mengine, jumla ya mada Nne zimewasilishwa.

Mada hizo ni pamoja na Umuhimu wa Maadili katika Utumishi wa Umma, Mabadiliko yaliyotokana na Kuunganishwa kwa Mifuko ya Pensheni, Utekelezaji wa Bajeti ya Tume kwa Mwaka 2019/20 na Mwelekeo wa Bajeti ya Tume kwa Mwaka wa Fedha 2020/2012.

Mada nyingine ni mwongozo wa kuandaa Ikama na Bajeti ya mishahara, kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 pamoja na mabadiliko mbalimbali ya miundo ya kiutumishi.