Home Habari CHUO CHA DIPLOMASIA KUPELEKA KISWAHILI ANGOLA

CHUO CHA DIPLOMASIA KUPELEKA KISWAHILI ANGOLA

352
0
Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Faraji Mnyepe wakiimba wimbo wa Taifa. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Chuo, Dkt. Jeremia Ponera.

Serikali imefurahishwa na Chuo Diplomasia, ambacho kimefikia hatua nzuri katika mpango wa kufundisha Kiswahili nchini Angola.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 22 ya Chuo hicho alisema, Rasimu ya Hati ya Makubaliano kati ya Chuo hicho na Chuo cha ISRI, cha Angola imeishaandaliwa, kinachosubiriwa ni kusainiwa.

Pia ili kufanikisha Sera ya Diplomasia ya Uchumi, Serikali imeagizwa Chuo hicho kutoa mafunzo kwa vitendo ili wahitimu wakidhi matakwa hayo ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki. Dkt. Faraji Mnyepe, akisoma hotuba yake kabla hajamkaribisha mgeni rasmi.

“Serikali itafurahi kusikia chuo kinatoa mafunzo ya stratejia, jiopolitiki na demokrasia pamoja na haki za binadamu hasa kwa muktadha wa kiafrika,” amesema Prof. Kabudi.

Amesema hatua hiyo itasaidia kufafanua masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa, yanayotokea duniani na ametaka uandaliwe mpango mkakati wa aina hiyo ya mafunzo, ili waone  jinsi gani Wizara itasaidia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), ambaye pia alikua mgeni rasmi wa Mahafali ya 22 ya Chuo cha Diplomasia, Dar es Salaam, akihutubi wakati wa mhafali yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho Kurasini Jijini Dar es Salaam.

“…, Chuo kipitie mitaala yake mara kwa mara kama ilivyopendekezwa, ili kisipitwe na wakati kwani dunia inabadilika kwa kasi, hatuna budi kwenda nayo sambamba,” amesema Prof. Kabudi.

Pia ametaka katika kutoa mafunzo hayo, Chuo hicho kitoe kipaumbele kwa wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na wafanyabiashara waliopo nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, amesema kati ya wahitimu 453 waliotunikiwa vyeti, 98 ni wa ngazi ya Astashahada ya msingi, 119 ni wa Stashahada ya kawaida, 130 ni wa Shahada, 83 ni wa Stashahada ya Uzamili na 45 Stashahada ya uzamili wa diplomasia ya uchumi.

Kwa mujibu wa Dkt. Mnyepe, katika mwaka wa masomo 2019/20 Chuo cha Diplomasia kimeongeza udahili wa wanafunzi, kutoka 1,029 kwa 2018/19 hadi 1,275 kwa mwaka wa masomo 2019/20 na kwamba juhudi za kupanua wigo wa udahili zinaendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), akimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi ambao wamefaulu vizuri masomo yao.

Amesema udahili mwingine utaanzishwa Machi mwaka huu, ikiwamo kuanzisha program mpya ambapo kwa Mwaka wa masomo 2019/2020, idadi ya program za muda mrefu imeongezwa huku Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Amani na Udhibiti wa Migogoro, ikiwa imeanzishwa.

Dkt. Mnyepe, amesema kwa sasa program hiyo inatolewa na Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam na Dodoma.