Home Habari DKT. BASHIRU AWASUTA “WANAOJIUZA” KWA MGONGO WA JPM; ATAKA WASIMCHAFUE RAIS

DKT. BASHIRU AWASUTA “WANAOJIUZA” KWA MGONGO WA JPM; ATAKA WASIMCHAFUE RAIS

349
0

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, ameshtukia janja ya baadhi ya wanachama hicho wanaojimwambafai, kwamba wanataka kugombea uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM-Taifa, ambaye pia ni  Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli.

Ikumbukwe, mwaka huu mwishoni utafanyika uchaguzi mkuu wa viongozi wa ngazi mbalimbali kitaifa, wakiwemo wabunge na madiwani.

“Ninafahamu Mwenyekiti hana mgombea yeyote, msimchafue hata mimi sina mgombea kwasababu watakaogombea nafasi mbalimbali za uongozi wote ni wa kwetu na wana haki sawa,” amesema Dkt. Bashiru.

Alikuwa kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, akipokea  taarifa ya kazi ya Mbunge wa Jimbo hilo, Peter Serukamba.

Amebainisha kuwepo baadhi ya wanachama ndani ya CCM, wanaolaghai wajumbe wa vikao kuwa wametumwa na mwenyekiti, katibu mkuu (yeye) au wazee kugombea.

Amewataka waache uongo na badala yake, wajiandae kueleze sifa zao na ajengda walizonazo katika kuwania nyadhifa hizo, kwakuwa ndiyo kanuni na mila za kugombea.

Rais, Dkt. Magufuli wakati akifanya kampeni kwenye uchaguzi mkuu uliyofanyika Mwaka 2015, alipogombea kiti cha urais wa Tanzania.

“Mwenyekiti (Rais, Dkt. Magufuli) hawezi kuwa na mgombea, hata yeye wakati anagombea hakusema ametumwa na yeyote, sifa zake zilimuuza kwa wapiga kura,” amesema Dkt. Bashiru.

Pamoja na mkutano huo wa kijimbo, Dkt. Bashiru amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Chankele – Mwamgongo, upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bitale na Kituo cha Utafiti wa mbegu za michikichi cha Kihinga.

Alifanya ziara hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM-Mkoa wa Kigoma, Amandus Nzamba, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Kirumbe Ng’enda, Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga na Wabunge; Daniel Nsanzugwako, Hasna Mwilima na Peter Serukamba.