Home Dodoma TAKUKURU YAMSWEKA NDANI AFISA MIFUGO KONGWA, MAAFISA WAWILI WA TRA DODOMA PIA...

TAKUKURU YAMSWEKA NDANI AFISA MIFUGO KONGWA, MAAFISA WAWILI WA TRA DODOMA PIA WAPANDISHWA KIZIMBANI

290
0

Ernest Emmanuel Mzungu (31) na Vincent Elias Hassan (29) maafisa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dodoma, wamekamatwa na Taasisi ya Kzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakituhumiwa kushawishi na kupokea rushwa ya Sh. Mil. 1 kutoka kwa mfanyabiashara Maliki Tarimo.

Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo amesema walichunguza na kulibaini kuwa Jumamosi, Januari 11 mwaka huu watuhumiwa walikamata wendesha mkokoteni kwa kuwa na mzigo wa alminium, huku risiti ya EFD aliyokuwa nayo ikiwa na tarehe za nyuma na isiyo na thamani halisi ya mzigo husika.

“Waliongozana na mwendesha mkokoteni akiwa na mzigo husika hadi dukani kwa Tarimo, maeneo ya Majengo-CCM, hawakumkuta hivyo waliacha namba yao ya simu na ujumbe wa kumtaka afike ofisini kwao TRA,” amesema Kibwengo.

Amesema walibaini pia kwamba kwa kutumia namba aliyoachiwa, Tarimo aliwapigia watuhumiwa simu ambao walimtaka awape kiasi hicho cha fedha, ili wasimchukulie hatua yeye na mteja wake.

Kibwengo alisema walichunguza zaidi na kubaini kuwa watuhumiwa waliuachia mzigo huo na wala ofisini kwao hawakupeleka taarifa yoyote, kuhusiana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa Kibwengo, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani jana.

Wakati huohuo; Afisa Mifugo Mwandamizi wa Halmashauri ya Kongwa, Dickson Festo Urio (52) ametiwa hatiani na Hakimu wa Mahakama  ya Wilaya ya Kongwa, Kisasila Sanguda, kwa makosa matatu yaliyyokuwa yanamkabili katika shauri la jinai namba 37 ya Mwaka 2018.

“Alikuwa anashitakiwa kwa kutumia risiti za kughushi, kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Sura ya 329 kwamba alinunua vifaa kwa ajili ya wafugaji,” amesema Kibwengo.

Urio amehukumiwa kifungo cha jela kwa miezi Sita au kulipa faini ya Sh. Laki Tatu (300, 000/=) kwa kila kosa na baada ya kutumikia adhabu hiyo, ameamriwa kuilipa Halmashauri ya Kongwa Sh. 1,638,000.