Home Dodoma KATIBU MKUU ALAT CHUPUCHUPU KUTUMBULIWA, KISA? MAJUNGU

KATIBU MKUU ALAT CHUPUCHUPU KUTUMBULIWA, KISA? MAJUNGU

442
0
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo.

 

MAJUNGU yaliyopikwa dhidi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), Elirehema Moses Kaaya, nusura yamsababishie kutumbuliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo.

Pona yake imetokana na uchunguzi uliofanywa kimya kimya na timu maalum iliyoundwa na Waziri Jafo, baada ya kupokea tuhuma mbalimbali dhidi ya Kaaya, ikiwemo madai kwamba ni mwizi wa vifaa vya ujenzi, katika miradi ya jumuiya hiyo.

Jafo amesema hayo Leo akizindua jengo la makao makuu ya ALAT jijini Dodoma, kwamba alipokea tuhuma nyingi dhidi ya Kaaya kiasi kilichosababisha aunde timu ya wataalam kuchunguza kabla hajamchukulia hatua.

(hakuwataja majina) Jafo amesema alifahamishwa na wapika majungu hao kuwa Kaaya, amekuwa akiiba hata ndoo zenye rangi, mabati kutoka katika miradi ya ujenzi na kusafirisha kwa kutumia basi la Machame.

“Mimi na wizi ni vitu viwili tofauti, nilishasema kuwa nisingezindua jengo hili na kama ningekuja, leo nilikuwa namtumbua huyu jamaa na kuagiza TAKUKURU wamchunguze,” amesema Jafo.

Amemshukuru Mungu kwa kumpa hekima na busara katika kushughulikia zengwe hilo, kwani amesema aliamua kuunda timu ya wataalamu kwa siri ili wachunguze nyendo za Kaaya katika utendaji wake.

Matokeo ya uchunguzi huo, yameelezwa naye kwamba yalimshtua kwasababu ilibainika kuwa Kaaya, alikuwa sawa na mwiba kwa baadhi ya watendaji wasiokuwa waadilifu.

“Tumegundua kuna watu walijaribu kulipa Sh. Mil. 7 kwa moja ya kazi zilizokuwa zinafanyika kwenye ujenzi wa jengo hili, lakini Kaaya ndiye alizuia wizi huo,”amebainisha Jafo.

Amewaasa viongozi wenzake kutofanya uamuzi wa haraka dhidi ya wanaowaongoza, pindi wanapopelekewa tuhuma dhidi yao badala yake, wachunguzi ili kuepuka kuumiza watumishi waadilifu.

Wapika majungu  kazini nao wametakiwa kuacha tabia hiyo mara moja, kwakuwa ni sawa na uuwaji.

“Mjue mnaposababisha mtumishi asiye na hatia kufukuzwa kazi, kuingia kwenye misukosuko, siyo peke yake anayeathirika, mnakuwa mmetesa watu wengi wanaotegemea mkono wake na dhambi hiyo haitawaacha salama,” amesema Jafo.

Amewaeleza wapika majungu hao kuwa adhabu ya dhambi wanayotenda, itawatafuna na vizazi vyao.

Ingawa hakutaja majina ya waliokuwa wakimpelekea uongo huo, Waziri Jafo amewanyooshea kidole watendaji ambao ni watumishi akisema baadhi yao wana shida kubwa, tofauti na madiwani ambao wameridhika na posho zao.

Uchunguzi wa sakata hilo umeelezwa naye kuwa umebaini mambo ikiwamo kiini cha zengwe hilo, kwamba ni nafasi ya Kaaya kazini na uadilifu wake.

Amemshukuru Kaaya kwa utendaji uliyotukuka na kumwomba aendelee kudhibiti raslimali za umma, akitimiza jukumu lake la kumuunga mkono Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  katika kukomesha wizi wa rasilimali.

Naye Kaaya akizungumza na EM Online amesema, alihisi kuzimia wakati Waziri Jafo akizungumzia tuhuma za uongo alizokuwa akipelekewa.

Amesema ingawa anafahamu kuna watu wasiopenda uwepo wake kwenye kazi anazofanya, hakujua kwamba anakabiliwa na vita kubwa kiasi kilichoelezwa.

“Kwakweli mikono yangu namnyooshea Mungu kumshukuru,  najua hataniacha kwasababu wanaonifitini wanakerwa na dhamira njema niliyonayo kwa Nchi yangu…,  sikujua nina vita kubwa kiasi hiki, sikujua nilikuwa nachunguzwa, siri wakati waziri anazungumza nilikuwa nahisi kuzimia ina maana leo ningefutwa kazi!?,” amezungumza Kaaya kwa masikitiko.

Kuhusu ‘dili’ la Sh. Mil. 7 amesema kuna kazi ambayo alitakiwa kuidhinisha ilipwe kiasi hicho cha fedha (bila kuitaja), akaamua kuifanyia ukaguzi na alipopata wasiwasi, akaomba ushauri kutoka kwa wataalam na kubaini kiasi halisi kilichotakiwa kulipwa ni kisichozidi Sh. Mil. 3.