Home Habari TANZANIA, NORWAY ZAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI NA BIASHARA

TANZANIA, NORWAY ZAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI NA BIASHARA

198
0

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba John Kabudi (Mb) amefanya majadiliano na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Norway kwa nchi zinazoendelea (NORFUND), Tellef Thorleifsson kuhusu fursa za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Norway.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo kwenye Ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam, Pro. Kabudi amesema Tanzania inafurahishwa na mradi wa Africado uliyopo Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro ambao unazalisha Maparachichi  yanayosafirishwa na kuuzwa nje ya Nchi.

Ametaja baadhi ya nchi yanakouzwa kuwa ni pamoja na Uholanzi, Uingereza, Ufaransa, Hispania, Ureno, na Mashariki ya Kati hali inayosaidia serikali kukuza pato lake la taifa na kwamba umetoa fursa za ajira takribani 600 kwa watanzania.

Naye Thorleifsson, amesema lengo la mfuko huo ni kuwekeza katika miradi mbalimbali ndani ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ili kuzisaidia kukuza uchumi.

Amesema hadi mwishoni mwa Mwaka 2018, mfuko huo ulikuwa umetumia Dola za Marekani Milioni 160, kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania katika sekta za Nishati, Fedha, Chakula na Kilimo.

Balozi wa Norway nchini, Ms. Elisabeth Jacobsen akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Norway (Norfund), Tellef Thorleifsson.

“Uwekezaji huu, umefanya Tanzania kuwa ya Nne katika nchi zinazonufaika na miradi ya Norfund,” amesema Thorleifsson.

NORFUND NI NINI?

Ni taasisi iliyo chini ya Serikali ya Norway, ambayo ina jukumu la kuwekeza mitaji na utaalamu katika kuanzisha miradi mbalimbali endelevu, kwenye nchi zinazoendelea ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.