Home Dodoma SERIKALI: TUTAENDELEA KUTAIFISHA MALI ZA WALA RUSHWA.

SERIKALI: TUTAENDELEA KUTAIFISHA MALI ZA WALA RUSHWA.

234
0
MKURUGENZI WA IDARA YA HABARI MAELEZO NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, DKT. HASSAN ABBAS, AKIZUNGUMZA KWENYE MKUTANO WAKE NA WANAHABARI JIJINI DODOMA LEO.

MSIMAMO wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika mageuzi ya kimfumo na kitaasisi, umesababisha Tanzania kuwa miongoni mwa vinara katika vita dhidi ya rushwa duniani.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema hayo akirejea utafiti uliyofanywa na Transparency International mwaka jana na kutangazwa Januari 23 Mwaka huu.

Amesema Tanzania imekuwa ya 96 duniani tofauti na Mwaka 2017 ilipokuwa ya 103 na ya 117 Mwaka 2015.

Kwa Afrika Mashariki Tanzana inatajwa na ripoti ya sasa kwamba ni ya Pili kwa kutokuwa na vitendo vya rushwa, ikitanguliwa na Rwanda.

Ametaka ikumbukwe katika kipengele cha juhudi za kupambana na rushwa, Julai mwaka jana Tanzania ilikuwa ya Kwanza kati ya Nchi 15 za Afrika, ambazo zilizofanyiwa utafiti na taasisi za Transparency na Afrobaramoter.

“Siyo siri kwamba haya ni mafanikio makubwa yanayotokana na msimamo wa Rais, Dkt. Magufuli katika vita hii ikiwemo kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuchukua hatua haraka hasa yanapotendeka makosa ya uhujumu uchumi,” amesema Dkt. Abbas.

Amesema Serikali katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa, imefikia hatua ya kutaifisha mali zote zinazothibitika kwa mujibu wa sheria kwamba zimetokana na rushwa.

Kwa mujibu wake, mali mbalimbali zikiwemo nyumba, magari na fedha taslim za waliothibitika mahakamani kuwa zilitokana na rushwa zimerudishwa serikali na kwamba hata msimamo wa Rais, Dkt. Magufuli hautabadilika katika suala hilo.

UTALII

WAWAKILISHI WA VYOMBO MBALIMBALI WA HABARI WAKIMSIKILIZA MKURUGENZI WA MAELEZO NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, DKT. HASSAN ABBAS.

Dkt. Abbas amesema matokeo ya serikali kuimarisha mifumo ya kodi, yaliyofanywa miaka mitatu iliyopita yamethibitisha kuwa wale waliodhani hatua hiyo ingesababisha watalii kukimbia hawakuwa sahihi kwasababu wameongezeka zaidi ya miaka iliyopita.

Amesema mwishoni mwa mwaka jana, hali ya watalii nchini ilionesha kuwa Mwaka 2018, Tanzania ilikuwa ya Nne Afrika kwa kuingiza Dola za Marekani Bilioni 2.43, kutoka Dola Bilioni 2.19 mwaka 2017, mapato yaliyotokana na utalii ikitanguliwa na Afrika Kusini, Misri na Morocco.

Shirika la Habari la CNN ya Novemba 2019 kupitia utafiti wa “Africa’s Most Amazing Places To Visit in 2020,” Dkt. Abbas amesema Tanzania ni ya kwanza hasa kutokana na vivutio, mandhari katika hifadhi ya Serengeti.

Dkt. Abbas alikuwa anazungumza na wananchi kupitia kwenye mkutano na vyombo vya habari jijini Dodoma, ikiwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kila mwezi.