Home Dodoma LEMA AWATAKA SIRO, SIMBACHAWENE, HAMDUN NA KATE WAJITAFAKARI. MWAKAJOKA ‘ALIA’ NA KUBAMBIKIWA...

LEMA AWATAKA SIRO, SIMBACHAWENE, HAMDUN NA KATE WAJITAFAKARI. MWAKAJOKA ‘ALIA’ NA KUBAMBIKIWA KESI.

224
0
WAZIRI KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, GODBLESS LEMA AKIZUNGUMZA KWENYE MKUTANO NA WANAHABARI JIJINI DODOMA LEO, PEMBENI YAKE KULIA NI MBUNGE WA TUNDUMA, FRANK MWAKAJOKA.

WAZIRI Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema (Mbunge wa Arusha mjini – Chadema), amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Salum Hamdun na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi, Joseph Kate wajiuzulu kufuatia vifo vya watu 20 na 16 kujeruhiwa mjini Moshi.

Amesema ingawa Kiongozi wa Kanisa la Calvary Assemblies Of God, Mtume Boniface Mwamposa inawezekana akashindwa kujiepusha na tukio hilo lakini, kiini cha tatizo ni kukosekana weledi katika kudhibiti mkusanyiko mkubwa wa watu, kama waliokuwa kwenye mkutano huo wa Ibada.

Ikumbukwe, vifo hivyo vimetokea Februali 01 Mwaka huu  kwenye uwanja wa Majengo, Halmashauri ya Moshi ambako waumini wa kanisa hilo, walitakiwa kukanyaga mafuta ya upako; wakakanyagana kiasi cha kusababisha madhara hayo.

“Mikutano ya kibunge kwetu wapinzani ikizidishwa hata dakika tano tu, askari hutushusha jukwaani na kututupa kwenye karandinga lao, iweje mkutano huu uliotakiwa kuisha Saa 12 jioni, uliendelea mpaka huduma ya kukanyaga mafuta ikaanza Saa 2:00 usiku na vifo tunasikia vilitokea kuanzia Saa 5:00 usiku?,” alisema Lema kwa kuhoji.

Akiambatana na Mbunge wa Tunduma – Chadema, Frank Mwakajoka kwenye mkutano na vyombo vya habari jijini Dodoma, Lema, amesema Polisi wangetimiza wajibu wao kwa kuhakikisha taratibu zote zinazotakiwa kuzingatiwa kwenye mkusanyiko mkubwa wa watu, madhara hayo yasingetokea.

Amesema serikali imekaririwa ikieleza kuwa mkusanyiko huo ulikuwa na watu wasiopungua 10,000.

Amesema haikutakiwa kukosekana watoa huduma ya kwanza, askari wa kikosi cha kuzima moto na uokoaji (fire) na askari polisi wa kutosha ili kuhakikisha usalama wa watu na mali unakuwepo.

Kwa mujibu wa Lema, hata kama mazingira hayakuwa mazuri kutolea huduma ya ukanyagaji wa mafuta, mamlaka za usalama zingekuwa makini ingewezekana kuzuia au kuelekeza namna nzuri ya kutoa huduma hiyo.

Amesema hata baada ya vifo hivyo kutokea, ilitarajiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Simbachawene, awajibishe waliotakiwa kutimiza wajibu huo lakini kwa kufumbia macho uzembe huo, naye hanabudi kujiuzulu.

Kwaupande wake Mbunge Mwakajoka, ametumia fursa hiyo kuwasilisha kilio chake kwa Rais, Dkt. John Magufuli, akimwomba atupie jicho jimboni Tunduma, akisema viongozi wengi wa Chadema wamebambikiwa kesi na polisi.

Amesema mpaka sasa chama hicho ndani ya Jimbo la Tunduma kina kesi 100, zinazoendelea kwenye mahakama ya mkoa, wilaya na za mwanzo.

Kwa upande mwingine amesema baadhi ya viongozi wa chama hicho, ngazi tofauti za jimbo pamoja na wenyeviti wa vijiji wapo mahabusu kwa muda mrefu sasa, baada ya kuundiwa mbinu zinazosababisha washindwe kukidhi vigezo wa kudhaminiwa.