Home Dodoma VIFO IBADANI: SERIKALI YAONA UMUHIMU WA MABADILIKO KTK KUSAJILI TAASISI ZA KIIMANI.

VIFO IBADANI: SERIKALI YAONA UMUHIMU WA MABADILIKO KTK KUSAJILI TAASISI ZA KIIMANI.

348
0

Kufuatia watu 20 kufariki kwa kukanyagana wakikanyaga mafuta ya upako, kwenye uwanja wa Majengo Manispaa ya Moshi, Serikali imesema kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko katika kusajili makanisa na taasisi za kiimani.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, GEORGE SIMBACHAWENE.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene pamoja na kutoa pole kwa wafiwa, amesema vibanda imani vimekuwa vingi kiasi ambacho ni muhimu viwekewe utaratibu.

“Kwa mfano Rwanda, ili mtu asajili kanisa lazima awe mwenye Shahada ya Theolojia lakini hapa kwetu suala hilo halipo,”amesema Simbachawene.

VIFO VILIVYOTOKEA

Kwa mujibu wa waziri, Mtume Boniface Mwaiposa almaarufu Brudoza wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, aliewa kibali cha kufanya mkutano wa Injili Januari 30 hadi Februali 01 Mwaka huu, Saa 6:00 mchana mpaka 12:00 jioni.

Jana, Februali 01 kati ya Saa 1:00 na Saa 2:00 usiku Mtume Mwaiposa alielekeza wafuasi wake ambao walikadiriwa kufikia 10,000 (Elfu Kumi), wapiti eneo lenye turubai lililotiwa mafuta, wakiaminishwa kuwa kwa kufanya hivyo wataondokana na matatizo waliyokuwa nayo.

Ni katika harakati za kutekeleza agizo hilo la kiimani, watu walikanyagana kiasi cha vifo hivyo kutokea huku wengine 16 wakijeruhiwa.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene, Mtume Mwaiposa na wasaidizi wake akiwemo aliyeomba na kupewa kibali cha mkutano huo, Elia Mwambamba wamekamatwa na Jeshi la Polisi.

Waziri amesema katika mazingira ambayo Mtume Mwamposa alikamatiwa, inasadikiwa alikuwa na nia ya kutoroka.

“Awali tulielezwa angeondoka Moshi kwa Ndege, lakini uwanja wa ndege tulimkosa mpaka alipokamatiwa Dar es Salaam, alfajiri ya Leo – Februali 02…, hii inatoa taswira kwamba alikusudia kutoroka,” Waziri alijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kama kuna ushahidi unaothibitisha kuwa Mwaiposa, alitoroka baada ya tukio.

KWANINI POLISI HAWAJAWAJIBISHWA?

Ingawa Waziri huyo amekiri kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha watu na mali zao wanakuwa salama, amesema:

Kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya Sura Namba 337 hasa kifungu cha 9 na 19, waziri wa mambo ya ndani ndiye anayesajili jumuiya hizi, za kijamii lakini pia madhehebu ya dini na shughuli zote za taasisi za watu binafsi.

Kwahivyo nina jukumu la kuhakikisha kwamba amani inakuwepo katika shughuli za taasisi hizo za kidini, ndiyo maana nimeona niseme na niwape pole sana familia hizi za watu 20 waliofariki na wale waliojeruhiwa.

Lakini lazima kama serikali tuchukue hatua stahiki.

Kwasababu inasikitisha kwamba una idadi kubwa ya watu, umewakusanya mahala, mwenye jukumu la kuhakikisha usalama wao ni wewe uliyewakusanya hapo.

Pamoja na jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba watu wanakuwa salama, lakini kwa idadi kubwa ya watu wa namna hiyo, unapotoa maelezo au maeneo ambayo yanaweza kusababisha mhemuko na watu wakaweza kukimbizana kufikia hatua ya kuumia basi una wajibu wa kuwajibishwa katika kosa hilo.

Kwahiyo nitoe rai kwa viongozi wa madhehebu na shughuli za kidini na mikusanyiko mbalimbali, kujua kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha usalama wa watu husika.

Kwanza kibali kilikuwa ni cha kutoka Saa 6:00 mchana hadi Saa 12:22 lakini tukio limeanza kufanyika kati ya Saa 1:00 na Saa 2:00 inaonesha jinsi ambavyo masharti ya kibali yalikuwa yamekiukwa.

Lakini kuwaelekeza watu zaidi ya 10,000 waliokusanyika kwamba wafike sehemu moja, pia inaonesha kutokuwajibika katika kuwa na dhamira ya kwamba unajua jukumu la kuhakikisha kwamba hao watu wanatakiwa kuwa salama.

Baada ya tukio Mtume Mwaiposa alitaka kukimbia na kutoroka, lakini mpaka sasa yupo mikononi mwa polisi, tunataka kumrudisha Moshi ili yeye pamoja na wenzake wakawajibike kwa madhara waliyosababisha.

Wengine wote wanaofanya shughuli kama hizo au kusababisha mikusanyiko, wahakikishe wanatumia maneno ambayo hayasababishi mihemko kwa waliowakusanya.