Home Dodoma KATIBU MKUU MPYA WA MAMBO YA NDANI AKABIDHIWA OFISI, AINGIA AKITAKA UWAZI...

KATIBU MKUU MPYA WA MAMBO YA NDANI AKABIDHIWA OFISI, AINGIA AKITAKA UWAZI NA UKWELI.

540
0

Na Mwandishi Wetu, MOHA, Dodoma.

KATIBU MKUU WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, CHRISTOPHER KADIO(KUSHOTO) AKIKABIDHIW OFISI NA ALIYEKUWA KAIMU KATIBU MKUU WA WIZARA HIYO, RAMADHAN KAILIMA, LEO JIJINI DODOMA.

KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima, amemkabidhi ofisi Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo, Christopher Kadio, jijini Dodoma leo.

Hiyo imefuatia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu kuandika barua ya kujiuzulu, Januari 22 Mwaka huu na kukubaliwa na Rais, Dkt. John Magufuli, baadaye baadaye alimteua kuwa Balozi.

Uteuzi huo ulitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. John Kijazi, Ikulu jijini Dar es Salaam, Januari 23 Mwaka huu.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Kidio amesema atakutana na kila mkuu wa Idara na kitengo ili kujua majukumu na changamoto zinazowakabili, kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

“Nataka mje tuzungumze, kila mmoja wenu aje ofisini kwangu tuzungumze, muwe wazi na wakweli ili nijue majukumu na changamoto zenu na tuweze kusaidiana,” amesema Katibu Mkuu.

KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI, CHRISTOPHER KADIO AKIZUNGUMZA NA BAADHI YA VIONGOZI WA WIZARA HIYO, KWENYE UKUMBI WA MIKUTANO WA WIZARA, JIJINI DODOMA LEO.

Ili kuleta mafanikio chanya kwa wizara na serikali kwa ujumla, amesema anataka wakuu hao wa idara na vitengo, kufanya kazi kwa ushirikiano.

“Nashukuru kwa kunikaribisha, nimefurahi kuwa nanyi, ila tufanye kazi kwa mashauriano ili tuweze kutatua changamoto mbalimbali ambazo kila Wizara wanazo pia nasi tunazo, “ alisema Kadio.

Kadio ameweka wazi kuwa ni muumini wa ukweli na uwazi katika utendaji kazi na ametaka watakaokutana naye, wasiwe na woga badala yake wawe wawazi na wakweli.

Safu ya juu ya uongozi wa Wizara hiyo ilifumuliwa na Rais, Dkt. Magufuli, kufuatia tuhuma za kuhusika na mkataba wenye kasoro ambao uliingiwa na Jeshi la Zimamoto.

Mkataba huo wa kununua ndege zisizokuwa na rubani, kwa ajili ya kuzima moto pindi inapotokea ajali ulielezwa kugubikwa na wingu la ufisadi.

Kasoro hizo ziliibuliwa na Rais, Dkt. Magufuli mwenyewe ambaye alitaja kila aliyehusika na alivyohusika, kabla hajaelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ruwa (TAKUKURU) kuwahoji.