Home Habari MMANGA AWAITA WANADODOMA KUSAIDIA WANAKILWA.

MMANGA AWAITA WANADODOMA KUSAIDIA WANAKILWA.

215
0
MKAZI WA JIJINI DODOMA, HASSAN MMANGA.

KUSAKA MKAZI wa Dodoma, Hassan Mmanga Suleyman, ameungana na uongozi wa Wilaya ya Kilwa, kuomba misaada kwa ajili ya wakazi wa vijiji 16 vya Wilaya hiyo, ambao wameathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua.

Mmanga mwenye asili ya Kilwa, Kata ya Miteja kijijini Ndalala ametoa wito huo akizungumza na EM Online, baada ya kurejea jijini Dodoma akitokea Kilwa, kufariji ndugu, jamaa na marafiki zake ambao wameathiriwa na janga hilo.

“Yaani ndugu zetu wana hali mbaya, kuna ambao hawana kitu chochote maana kila kilichokuwa chao ikiwamo makazi, vimesombwa na maji, mwenye chochote ajitolee kusaidia ili angalau kuwapunguzia maumivu,”amesema Mmanga.

Ameomba aliye tayari kusaidia katika hilo, kwa namna yoyote ile na ambaye yupo Dodoma, awasiliana naye kwa namba ya simu 0655984894 ili ampe mwongozo.

MKUU WA WILAYA YA KILWA, CHRISTOPHER NGUBIAGAI.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christorpher Ngubiagai, alisema takriban watu 15,096 kutoka kaya 3,774 wameathiriwa na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua, iliyonyesha kwa siku tatu, mwishoni mwa mwezi uliyopita.

Uokoaji umekamilika, kwa sasa serikali ya wilaya hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Lindi, imejikita katika kuwezesha wananchi, kupata huduma na mahitaji ya kujikimu

Ngubiagai ametoa wito kwa yeyote aliyeguswa, mwenye chochote kinachoweza kusaidia wananchi hao, ajitokeze ili washirikiane.

“Tunahitaji mablaketi, mashuka, nguo, sabuni, nguo, vyombo mbalimbali, vyakula, sale za wanafunzi, daftari, kalamu, yaani kila kitu kinahitajika, waswahili husema kutoa ni Moyo siyo utajiri, naomba wananchi wote mjitolee kutusaidia katika hili,” amesema.

DC ameelekeza kuwa mwenye chochote anaweza kutoa kupitia ofisi yake (DC-Kilwa), Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa hata kwenye Ofisi za watendaji wa kata na vijiji na kuomba ifahamike kuwa hakuna zawadi ndogo, watapokea chochote kitakachopatikana.