Home Dodoma HOSPITALI YA MACHO YA CVT, INAVYOADHIMISHA SIKU YA WAPENDANAO

HOSPITALI YA MACHO YA CVT, INAVYOADHIMISHA SIKU YA WAPENDANAO

422
0

SIKU ya Wapendanao almaarufu Valentine’s Day, huadhimishwa Februari 14 kila mwaka.

Mara nyingi, mtu na mtu hufanyiana mambo mazuri, ili kuachiana kumbukumbu za upendo, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo.

Hospitali ya Macho ya CVT kwa awamu ya Pili tangu ilipoanzishwa Mwaka 2018 inafanya maadhimisho hayo kwa kampeni inayoitwa Onesha Upendo.

Hospitali hiyo inayofahamika kwa jina la CVT EYE HOSPITAL, ipo Mtaa wa Kilimani jirani na mabweni ya Furaha ya Chuo Cha Mipango, uelekeo wa Klabu ya Waswanu (Waswanu Pub) ukiwa unatokea katikati ya Jiji la Dodoma.

Meneja wa Hospitali hiyo, Lulu Mollel, kupitia mazungumzo maalum na EM Online amesema kampeni hiyo kama ilivyokuwa mwaka jana, mwaka huu imeanza kutekelezwa tangu Februali 01.

“Ingawa tunahudumia wagonjwa wote wenye maradhi ya macho na kuwapatia tiba, tumejikita zaidi katika kuhudumia wenye maradhi ya mtoto wa jicho na wanaobainika kuhitaji tiba ya upasuaji tunawafanyia,” amesema Lulu.

Wanaokutwa na maradhi ya mtoto wa jicho, wengi ni wazee wenye umri wa kati ya miaka 60 na 90.

Vijana na watoto wanaokutwa na tatizo hilo, mara nyingi inakuwa imesababishwa na ajali, zinazowapata katika mazingira tofauti.

“Onesha Upendo” Inavyomnufaisha Mgonjwa.

MMOJA WA WANUFAIKA WA KAMPENI YA ONESHA UPENDO, AKIFUATA MWONGOZO WA KUCHUNGUZWA MACHO.

Lulu amesema kampeni hiyo inafuta gharama kwa baadhi ya huduma na kupunguza sana gharama kwa huduma nyingine.

Kwamfano gharama za kuhudumiwa na daktari ni Sh. 15,000 lakini wakati wa kampeni huduma hiyo inatolewa bure.

Kufanyiwa upasuaji ili kutoa mtoto wa jicho hugharimu Sh. 300,000 (laki tatu) lakini wakati wa kampeni kwa mwaka huu ni Sh. 50,000 (elfu hamsini).

Amesema mwaka huu wataalam wamewafata wagonjwa kwenye Wilaya za Kongwa, Chemba, Kondoa TC na Dodoma mjini.

Watakaobainika kuhitaji upasuaji ili kuondolewa mtoto wa jicho, watasafirishwa kupelekwa hospitalini siku ya kufanyiwa upasuaji na kurudishwa walipochukuliwa baada ya kutibiwa.

Lengo ni kufikia maeneo yote lakini kwingine kutafikishiwa huduma, kadiri nyenzo wezeshi zitakavyopatikana.

Gharama za Kutekeleza Kampeni hii Zinapatikana Wapi?

Shirika la CVT ni miongoni mwa hospitali zaidi ya 16 nchini, zenye watalam wa upasuaji wa mtoto wa jicho ambazo zinafadhiliwa kwa kupewa bure vifa tiba vya upasuaji.

Ameishukuru Serikali kuu kwa kubariki shughuli hizo na kuwapa miongozo inayowasaidia kuzifanikisha.

“Kupitia katibu tawala wa mkoa na RMO (Mganga Mkuu wa Mkoa) Serikali ya Mkoa inatupa ushirikiano wa kutosha hata ma DMO (waganga wakuu wa wilaya) katika maeneo tunayofanya kampeni hii wamekuwa msaada mkubwa kwetu,” amesema Lulu.

Amewashukuru na viongozi wa dini wa madhehebu yote ya Kikristo na Kiislam, kwa kuwatangazia waumini wao kuhusu uwepo wa  huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.

Naye Mratibu wa Macho Tanzania, Dkt. Bernadetha Shilio, ametajwa kuwa anawasaidia katika kufanikisha shuguli hizo, hasa kwa kuwaongoza kufikia hospitali zenye uhitaji.

Tangu Februali 01 hadi Februali 01 Mwaka huu amesema wanafanya vipimo vya macho na kutoa tiba za kawaida, hospitalini pamoja na kwenye wilaya ambazo wamepeleka wataalam wao.

Wanaotakiwi kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutolewa mtoto wa jicho, amesema wanaandaliwa kwa ajili hiyo na huduma itakayofanyika kuanzia Februali 11 hadi Februali 14.

Yaliyojiri Katika “Onesha Upendo” Mwaka jana

Amesema mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji kwa ajili ya kufanyiwa tiba ya mtoto wa jicho alilipa Sh.100,000.

Kila siku walifanyia uchunguzi takriban watu 100 na mpaka kilele cha kampeni hiyo, watu 2,000 walifanyiwa uchunguzi na kupewa tiba mbalimbali huku zaidi ya watu 100 wakifanyiwa upasuaji kuondolewa mtoto wa jicho.

Huduma Nje ya Onesha Upendo

Amesema wanatoa huduma zote za matibabu ya macho na ni miongoni mwa hospitali zinazohudumia watu waliojiunga na mifuko ya bima za afya.

Gharama za upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho ni Sh. 300,000 na kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi ni Sh.15, 000.

Hata hivyo amesema baadhi ya wagonjwa wanaotakiwa kutolewa mtoto wa jicho, kutokana na sababu mbalimbali hulazimika kuhudumiwa kila mwisho wa mwezi, kwa gharama ya Sh. 100,000 (laki moja) baada ya kuchunguzwa na daktari.

Tofauti na kipindi cha kampeni ambapo huduma hutolewa kila Jumatatu Saa 1:00 asubuhi hadi Jumamosi Saa 11:00 jioni, hospitali hiyo hutoa huduma zake Jumatatu Saa 1:00 asubuhi hadi Jumamosi, Saa 7:00 mchana.