Home Habari SERIKALI YAPELEKA ZAIDI YA BIL.1/- ARUSHA

SERIKALI YAPELEKA ZAIDI YA BIL.1/- ARUSHA

222
0

NA MWANDISHI WETU,
ARUSHA.
Wananchi wa vijiji vya Oldonywas, Mbuyuni na Nduruma katika Halmashauri ya Arusha wamejitolea kuchangia nguvu zao ili kutekeleza miradi ya afya na elimu ambayo serikali imeipatia zaidi ya Sh. Bilioni Moja.

Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Arusha, Zelothe Stevene, imetembelea jumla ya miradi mikubwa mitatu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka minne, tangu serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa, serikali ya awamu ya tano imefanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo nchini kwa kufanikiwa, kutekeleza miradi mingi kisekta, kwa muda mfupi, kulinganisha na awamu zilizotangulia, miradi ambayo imeleta mabadiliko makubwa kwa jamii, ususani wananchi waishio vijijini.

“Nimeridhishwa sana na taarifa za miradi yote iliyotembelewa na Kamati yangu ya Siasa na kuona wananchi wakiwa wamechangia utekelezaji wa miradi hiyo kwa zaidi ya asilimia 10, jambo ambalo miaka ya nyuma ilikuwa changamoto, hii inaonyesha wazi wananchi wametambua na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano,” amesema Mwenyekiti Steven

Hata hivyo Mwenyekiti huyo, ameainisha miradi ya elimu na afya iliyotembelewa na kamati yake, ni pamoja na upanuzi wa Kituo cha Afya M’buyuni kata ya oljoro, uliogharimu shilingi milioni 400, upanuzi wa Kituo cha Kituo cha Afya Nduruma shilingi milioni 500 na ujenzi wa shule mpya ya Oldonyowas iliyo gharimu shilingi milioni 709.3.

Ameongeza kuwa vituo hivyo kwa sasa, vimeanza kutoa huduma sasa 24, ikiwa ni huduma ya kulaza, huduma ya upasuaji, huduma za kujifungua, maabara, pamoja na huduma za mama na mtoto, jambo ambalo litapunguza vifo visivyo vya lazima, hususani vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, ikiwa ndio uhalisia wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Edward kivuyo ni mwananchi wa kijiji cha Mbuyuni, amesema kuwa wanajivunia maendeleo yaliyo letwa na Rais Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano, kwa kujenga kituo cha afya, kituo kilichowapunguzia adha ya kufuata huduma zaidi ya Kilomoira 40, adha ambayo ilisababisha wajawazito kujifungulia, nyumbani, wengine njiani wakienda hospitali, na wengine kupoteza maisha yao na watoto wao.

“Kituo hiki cha afya ni historia, hajawahi kutokea Oljoro, wanawake wengi walikua wanajifungulia nyumbani, wengine njiani kwa sababu ya umbali wa kituo cha afya, tumepoteza kinamama na mtoto wakati wa kujifungua, lakini kwa sasa tunajivunia maendeleo ya serikali yetu ya awamu ya tano kwa kutujengea kituo cha afya” amesema Kivuyo.

Kamati hiyo imetembelea ujenzi wa majengo ya Upasuaji, maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mganga kituo cha Afya Nduruma.

Ujenzi mwingine ni nyumba ya mganga kituo cha Afya Mbuyuni, ujenzi wa vyumba vya madarasa, jengo la utawala, maabara za masomo ya sayansi, mabweni mawili ya wasichana na nyumba mbili za walimu, shule ya sekondari Oldonyowasi.