Home Dodoma MENEJA WA TANESCO KANDA YA KATI, ENG. TEMU, AKWEA KIZIMBANI LEO.

MENEJA WA TANESCO KANDA YA KATI, ENG. TEMU, AKWEA KIZIMBANI LEO.

564
0

MENEJA wa Tanesco Kanda ya Kati, Mhandisi Zakayo Godfrey Temu, leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Dodoma, Paschal Mayumba, akiwa shahidi wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kesi ya kuchoma moto nyumba, unayomkabili Christophe Kione (24).

Mhandisi Temu, ametoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Paschal Mayumba, katika kesi hiyo ya jinai Na. 190/2019.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Salma Uredi, Mhandisi Temu ameieleza mahakama kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Dodoma, jukumu lake kuu likiwa kusimamia usambazaji na uuzaji wa umeme mkoani humo.

Amedai kuwa Septemba 02 Mwaka jana, alipokea barua kutoka kwa mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Dodoma ikiwataka kuchunguza tukio la kuungua nyumba, iliyoko eneo la Makole.

Naye aliwaagiza wataalamu wa shirika hilo, kufanya uchunguzi wa kuungua kwa nyumba hiyo, ambao walimpelekea taarifa za uchunguzi ambazo zilipelekwa kwa mkuu wa upelelezi wa wilaya, kwa maandishi.

“Miundombinu ya Tanesco; ikimaanisha mita na njia ya kupeleka umeme kwenye nyumba husika ilikuwa salama kabisa, matokeo ya uchunguzi yalipelekwa kwa mkuu wa upelelezi wa wilaya kwa barua ya Septemba 04, 2019,” ameeleza Mhandisi Temu.

Barua hiyo yenye sahihi ya Mhandisi Temu, imewasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Uredi, kama kielelezo namba Tano.

Naye mshitakiwa, Kione, alipopewa nafasi ya kumuuliza shahidi maswali ilikuwa hivi:

Kione: Shahidi umeieleza mahakama kuwa ulituma wataalamu kuchunguza eneo la tukio, hiyo inamaanisha haukufika eneo la tukio?

Mhandisi Temu: Ndiyo, nilituma wataalamu.

Kione: Kwahiyo unachokieleza mbele ya mahakama ni taarifa ulizoletewa; Kwanini waliokwenda kuchunguza tukio wasiletwe kutoa ushahidi, badala yake uje wewe?

Mhandisi Temu: Wito ulioletwa ofisini ulinitaja mimi, siyo jukumu langu kupanga nani aje mahakamani, ikionekana inafaa waje hao unaowasema, watakuja wakiitwa.

Kione: Kama nimekuelewa vizuri, umeieleza mahakama kwamba uchunguzi wenu uliishia kwenye mita na njia ya kuingizia umeme ndani ya nyumba husika, Je, unajuaje ikiwa moto ulitokana na Pasi iliyoachwa ikiwaka?

Mhandisi Temu: Ushahidi ninaotoa hapa ni wa kitaalamu, kwenye matukio ya nyumba kuungua Tanesco jukumu letu linaishia kwenye miundombinu yetu kwa maana ya mita na njia ya kuingizia umeme kwenye jengo, baada ya hapo yanayoendelea ndani ya jengo yanamhusu mwenye jengo (mteja).

Ndiyo maana hata kwenye barua tuliyomwandikia mkuu wa upelelezi wa wilaya, tukijibu barua yake iliyotutaka kufanya uchunguzi tulieleza hilo na tukataka uchunguzi wao uendelee ili kubaini chanzo cha ajali husika, kwasababu miundombinu yetu kwenye nyumba ile ilikuwa salama.

Kione: Je, una kielelezo chochote cha kuionesha mahakama kuwa nyumba husika iliungua moto?

Mhandisi Temu: Ni barua tuliyoandikiwa na tuliyojibu kuhusiana na tukio hilo.

Kione anashitakiwa kwa kuchoma moto nyumba iliyopo Makole, alimokuwa anaishi dada yake – mtoto wa mama yake mkubwa anayefahamika kwa jina la Situmai Musa, ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo.

Pamoja na Situmai, mashahidi wengine wa Jamhuri ambao wameishatoa usahidi mbele ya mahakama hiyo ni Daniel Chaula, Catherine Mathias, Shadya Moyo na Emmanuel Ochieng.

Mashahidi wengine wawili wanatarajiwa kuendelea kutoa ushahidi.

Aidha, Hakimu Mayumba ameagiza barua za wito wa mahakama zipelekwe kwa mashahidi waliobakia na kumuagiza Wakili wa Serikali, Salma Uredi kumpa Kione nakala ya maelezo ya mlalamikaji kwakuwa ni haki yake.

Kesi imeahirishwa na Hakimu huyo mpaka Februali 25 Mwaka huu, itakapokuja tena kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashahidi. Mshitakiwa anaendelea kubaki rumande.

Ikumbukwe, Kione, kabla ya tukio hilo alikuwa Askari wa Kikosi cha Kuzuia ghasia cha Mkoa wa Dodoma (FFU).